Friday 2 May 2014

MAGONJWA SUGU YASIYO YA KUAMBUKIZA ILI UJIEPUSHE NAYO-3

 
 
Ugonjwa wa saratani
Saratani ni ugonjwa unaotokana na seli za mwili zilizopoteza mfumo wake wa kugawanyika na hivyo hazipo katika hali yake ya kawaida. Seli huweza kugawanyika bila mpangilio maalum na kuharibu mkusanyiko wa seli nyingine. Seli za saratani hutokea sehemu moja ya mwili na zinaweza 
 
kusambaa sehemu nyingine za mwili, saratani pia husababishwa na hali ya mazingira ya vitu mbalimbali kama vile ulaji wa vyakula vyenye visabbishi vya saratani (carcinogenic compounds), ulaji usiofaa, unywaji wa pombe, uvutaji sigara au minoni hatari, “asbestos” lisasi (lead), uranium na zebaki.
 
 
Zipo pia baadhi ya saratani zinazosabishwa na virusi kama  
 
hepatitis B  
ambayo huleta saratani ya ini na human papiloma inahusishwa na saratani ya shingo ya kizazi. Saratani huweza kutokea kwenye sehemu mbalimbali za mwili kama vile mapafu, matiti ovary, kibofu cha mkojo, shingo ya uzazi, utumbo, koo, kinywa, tezi dume (prostate), ini na ngozi.
 
Ulaji unaofaa na mtindo bora wa maisha ni vigezo muhimu sana katika kuzuia saratani na pia ni sehemu muhimu ya matibabu na kudumisha maisha bora baada ya kupata matibabu. Matumizi ya baadhi ya vyakula huweza kuongeza uwezekano wa kupata saratani. Uzito wa mwili ukiwa mkubwa unaweza pia kuongeza uwezekano wa kupata baadhi ya saratani Ni muhimu kufuata mtindo bora wa maisha kwani ni bora kuzuia kuliko kutibu.
 
Mambo yanayohusiana na mtindo wa maisha yanayoweza kuchangia katika 
kupata saratani.
Tafiti zinaonesha kwamba saratani za kurithi ni chache sana ila saratani nyingi hutokana na sababu za kimazingira. Tafiti nyingi zimeonesha kuwa kiasi cha asilimia 40 hadi 60 za saratani husababishwa na mtindo wa maisha usiofaa hasa ulaji usiofaa na kutofanya mazoezi ya mwili. Mtindo wa maisha usiofaa unajumuisha:
Ulaji wa vyakula vyenye nishati-lishe kwa wingi ambavyo husababisha unene. Unene umeonekana kuhusiana na saratani ya mji wa uzazi, matiti, figo, tezi dume, utumbo mpana na kibofu cha mkojo;
·        Ulaji wa nyama nyekundu kwa wingi na zile zilizosindikwa vimehusishwa na saratani ya tezi la kiume, utumbo mpana, mapafu, kinywa na koo;
·        Utumiaji wa pombe kwa wingi huongeza hatari ya kupata saratani ya mdomo, koo, koromeo, utumbo mpana, kongosho, ini na matiti;
 
Ushauri wa chakula na lishe wa jinsi ya kukabiliana na matatizo ya kiafya yanayoambatana na kuwa na saratani au tiba yake:
Matatizo mbalimbali yanaweza kujitokeza kutokana na hatua ya ugonjwa au aina ya matibabu mgonjwa anayopata, hasa dawa za saratani (chemotherapy) au mionzi. Matatizo hayo ni kama kukonda, upungufu wa damu, kukosa hamu ya kula, kichefuchefu, kutapika, kuhara, kukosa choo, vidonda kinywani, na matatizo ya ngozi.
Kukonda
Wagonjwa wengi wa saratani wanapungua uzito wakati wa matibabu. Hii inaweza kusababishwa na madhara ya saratani yenyewe, ongezeko la mahitaji ya virutubishi mwilini, kukosa hamu ya kula, aina ya matibabu anayopata mgonjwa (dawa, mionzi au upasuaji). Yafuatayo huweza kusaidia katika kukabiliana na tatizo hili:
·        
 Kuzingatia ulaji wa mlo kamili na ulaji wa aina mbalimbali za vyakula;
·        Kuongeza ulaji wa vyakula vyenye protini kwa wingi yenye asili ya wanyama (isipokuwa nyama nyekundu) na mimea.
·        Kula vyakula vilivyo laini vilivyoboreshwa na kuongezewa vyakula vyenye protini na nishati-lishe kwa wingi.
·        Kula milo midogo midogo mara kwa mara na kuongeza asusa zenye virutubishi vingi;
·        Kujitahidi kula wakati una hamu yakula au ukiwa na njaa kali na kula vyakula vile vyenye virutubishi kwa wingi;
·        Kufanya mazoezi kabla ya kula (kama vile kutembea) ili kuongeza hamu ya kula na kusaidia uyeyushwaji wa chakula;
·        Kula taratibu, usile kwa haraka bali jipe muda wa kutosha wakati wa kula;
·        Kutumia viungo vyenye harufu unayoipenda
·        Kutumia vinywaji kati yam lo na mlo na sio wakati wa kula kuepuka tumbo kujaa na hivyo kushindwa kula chakula cha kutosha; na
·        Kutumia vinywaji vyenye virutubishi vingi na nishati-lishe.
 
JINSI YA KUZUIA AU KUPUNGUZA MAGONJWA SUGU YASIYO YA KUAMBUKIZA
Magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza yanaweza kuzuiwa au kupunguzwa kwa kufuata mtindo bora wa maisha. Mtindo bora wa maisha ni muhimu katika 
 
kuendeleza na kudumisha afya ya mtu na kuzuia maradhi, hususani magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza.Mtindo bora wa maisha ni ule unaozingatia ulaji unaofaa, kufanya mazoezi ya mwili, kuepuka matumizi ya sigara na bidhaa zitokanazo na tumbaku, kuepuka matumizi ya pombe, na kuepuka msongo wa mawazo.
Ulaji unaofaa:
Ulaji unaofaa hutokana na kula chakula chenye mchanganyiko wa angalau chakula kimoja kutoka katika makundi matano ya vyakula na kupunguza kiasi cha mafuta, chumvi, na sukari kinachotumika.
 
Ulaji unaofaa unatakiwa kuzingatia mahitaji ya mwili kutokana na jinsi, umri, mzunguko wa maisha (mfano utoto, ujana, uzee), hali ya kifiziolojia (mfano ujauzito, kunyonyesha), kazi au shughuli na hali ya afya.
Ulaji unaofaa huchangia katika kudumisha uzito wa mwili unaotakiwa na kupunguza maradhi, yakiwemo magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza.
 
Mambo ya kuzingatia ili kufanikisha ulaji unaofaa:
• Kula mlo kamili mara tatu kwa siku.
• Kula matunda na mboga mboga kwa wingi kila siku.
• Kula vyakula venye makapi mlo kwa wingi.
• Epuka kutumia sukari nyingi.
• Epuka kula vyakula venye chumvi nyingi.
• Kunywa maji safi, salama na ya kutosha
• Kula asusa zilizo bora kilishe.
 
Kufanya mazoezi ya mwili :
Ni muhimu kwa binadamu wote, mtoto au mtu mzima, mnene au mwembamba, mgonjwa au mwenye afya njema kufanya mazoezi kwani husaidia mifumo mbalimbali ya mwili kufanya kazi kwa ufanisi. Mazoezi hupunguza uwezekano wa kupata saratani, ugonjwa wa kisukari, magonjwa ya moyo, na shinikizo kubwa la damu.
 
Mazoezi husaidia pia katika kuzuia ongezeko la uzito wa mwili, kupunguza msongo wa mawazo, na pia huboresha afya ya akili ikiwa ni pamoja na kuboresha uwezo wa kufikiri, kuelewa na kukumbuka. Inashauriwa kufanya mazoezi ya mwili angalau kwa dakika 30 kila siku, yaani mazoezi yanayotumia nguvu kiasi kama kutembea kwa haraka.
 
Anza kwa kutembea kwa muda mfupi, na baadaye unaweza kuongeza muda hadi dakika 60 kila siku, ukishindwa kabisa kufanya kila siku fanya angalau dakika 60 mara tatu kwa wiki.
 
kuepuka matumizi ya pombe:
Pombe husababisha ongezeko la uzito wa mwili ambalo linahusishwa na magonjwa mengi sugu yasiyo ya kuambukiza. Tafiti zimethibitisha kwamba pombe inaongeza sana uwezekano wa kupata saratani hasa ya mdomo, koo, koromeo, matiti, utumbo mpana na ini.
 
Tafiti zimeonyesha kwamba pombe ina madhara mengikiafya, ikiwa ni pamoja na kusababisha magonjwa, kupunguza uwezekano wa ini kufanya kazi vizuri, na pia huathiri uwekaji wa virutubishi mwilini.
 
Endapo unakunywa pombe kwa mwanaume inashauriwa kunywa vipimo viwili ambavyo ni sawa na milimita 500 za bia, mvinyo milimita 200, na pombe kali milimita 50 kwa siku . Kwa mwanamke anashauriwa kunywa nusu ya vipimo vinavyotumika kwa mwanaume.
Kuepuka matumizi ya sigara na bidhaa nyingine za tumbaku:
Uvutaji wa sigara, utumiaji wa tumbaku na bidhaa zake huongeza uwezekano wa kupata ugonjwa wa moyo, saratani ( hasa za mapafu, kinywa na koo), magunjwa sugu mengine ya njia ya hewa, shinikizo kubwa la damu na 
 
vidonda vya tumbo hivyo ni muhimu kuepuka.
Sumu aina ya nikotini iliyopo katika sigara huharibu ngozi ya ndani hivyo huongeza uwezekano wa lehemu kujikusanya kwenye sehemu za mishipa ya damu zilizoathiriwa.
 
Nikotini pia huweza kusababisha mishipa ya damu kuziba au kuwa myembamba kuliko kawaida na hivyo kuzuia damu kupita inavyotakiwa . Matumizi ya sigara pia huweza kuleta athari kwa wale walio karibu na mvutaji hususani kwa mama mjamzito na mtoto.
 
Kuepuka msongo wa mawazo
Msongo wa mawazo ni hisia ambayo huweza kuamshwa na matukio mbali mbali kama vile kufiwa na mtu wa karibu, kukabiliwa na tatizo katika( familia,maisha au shuleni), kuwa na kazi nyingi kwa muda mrefu bila ya kuwa na muda wa kupumzika. Hisia hizo zinaweza kusababisha hasira, wasiwasi, woga, huzuni, kuchanganyikiwa na pia kukata tamaa. Msongo wa mawazo ukijitokeza mara kwa mara huweza kusababisha ulaji usiofaa na mifumo ya mwili kutofanya kazi vizuri
Inashauriwa kupunguza msongo wa mawazo kwa kufanya mazoezi, kujipa muda wa kupumzika, kushiriki katika shughuli mbali mbali kama michezo, matamasha, harusi, na pia kupangilia vizuri jinsi ya kutumia muda wako. Jadili na mtu unayemwmini kuhusu matatizo yako, cheka au angua kilio, zima simu yako kwa muda katika siku.
HITIMISHO
Watu wengi tunakumbwa na magonjwa haya kutokana na kuwa na mtindo wa maisha usiofaa, ni vyema kuzingatia mtindo bora wa maisha ili kupunguza uwezekano wa kupata magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza.
USHAURI
·        Ni vyema kushiriki katika michezo, na mazoezi ya viungo.
·        Ni muhimu kujenga mazoea ya kupima mara kwa mara afya zetu.
·        Tuzingatie mtindo bora wa maisha ili kuzuia au kupunguza uwezekano wa kupata magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza.

0 comments:

Post a Comment