Saturday 3 May 2014

JE UNAJUA AFYA NI NINI?




Wapenzi wasomaji wa makala zangu ni matumaini yangu kuwa hamjambo popote pale mlipo mkiwa mnazisoma makala hizi za afya.

Nimeamua leo kuzungumzia mada inayohusiana na Afya kwa ujumla. Najua ungependa kwanza tuwaeleweshane Neno   'afya' linamaanisha nini hasa.

AFYA Kwa mujibu wa  ufafanuzi uliotolewa na kutangazwa na Shirika la Afya Duniani WHO katika mkutano wake wa tarehe 19-22 Juni 1946 na kusainiwa na wawakilishi wa nchi 61 duniani, Ni kuwa
 
 'afya ni hali ya mtu kuwa vizuri kimwili, kiakili na kijamii na sio tu kutokuwa na ugonjwa au udhaifu.' Ufafanuzi huo ulianza kutumika Aprili mwaka 1948 na hadi hii leo
maana hiyo ya afya haijabadika.


Ufafanuzi huo unamaanisha kwamba, tunaposema mtu ana afya sio tu tunakusudia kuwa mwili wake hauna maradhi, upungufu au udhaifu bali pia mtu huyo anatakiwa asiwe na 
 
matatizo ya kimwili, kiakili na hata kijamii. Kwa mujibu wa maana hiyo pana ya neno 'afya' tunaona kuwa watu wengi wanaamini kuwa afya imeganyika katika makundi mawili muhimu ambayo ni afya ya kimwili na afya ya kiakili.

 
Afya ya mwili kwa binaadamu ina maana, kuwa na mwili wenye afya usiokuwa na maradhi, afya ambayo kwa kawaida hutokana na kuupa mwili mazoezi ya mara kwa mara, lishe bora na mapumziko ya kutosha.

Katika nchi au maeneo ambayo watu wanapata lishe bora, huduma nzuri za afya na kuishi katika hali ya kimaisha 
 
inayoambatana na viwango vinavyotakiwa, kwa kawaida vimo na uzito wao huongezeka. Ukweli ni kuwa, ukiwauliza watu wengi afya ni nini, watasema kwamba inahusiana na  mwili kuwa salama bila ya kuathirika na ugonjwa.
Lakini tukienda ndani zaidi, kitiba afya ya mwili 
 
inaamanisha ustawi wa mwili hali ambayo mtu anaipata kwa kutekeleza vipengee vyote vinavyohusiana na afya katika maisha yake.
 
Uzima wa mwili unaakisi kufanya kazi vizuri moyo na mfumo wa kupumua, uwezo wa misuli, viungo pamoja na mwili kuweza kukubali mabadiliko tofauti na muundo wa mwili kwa ujumla.
 
Masuala mengine ni pamoja na lishe bora, uzito wa mwili, kutokuwepo uraibu wa madawa ya kulevya, pombe, mahusiano salama ya kimwili, usafi kwa ujumla na pia kulala na kuamka kwa wakati unaotakiwa.

Afya ya akili au uzima wa kiakili ni utambuzi wa mtu na uzima wake kisaikolojia. Mtu ambaye ana afya nzuri ya kiakili hana matatizo ya kiakili au kichaa. Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani WHO, 'afya ya akili ni pale mtu anapoweza kufahamu uwezo wake na kustahamili 
 
mfadhaiko (stress) unaotakana na dhiki au matatizo ya kawaida ya kimaisha. Aweze kufanya kazi yenye kuleta mafanikio na kuchangia masuala tofauti katika jamii yake.'
 
Ni rahisi watu kuelezea maana ya ugonjwa wa akili kuliko afya ya akili. Watu wengi wanakubali kwamba afya ya akili ni kutokuwepo ugonjwa wa akili lakini maana hiyo haitoshi. 
 
Hii ni kwa sababu kama tutachagua watu 100 ambao hawana kichaa au ugonjwa wa akili unaoweza kutambuliwa na daktari wa akili, lakini miongoni mwao tunaweza kuona kwamba afya ya baadhi yao kiakili imeimarika kuliko wengine.
Tunaweza kusema kuwa, afya ya akili inajumuisha masuala kadhaa kama vile uwezo wa kuishi kwa furaha, uwezo wa 
 
kuvumilia shida na kurejea katika hali ya kawaida baada ya kupatwa na matitizo, uwezo wa kuwa na uwiano katika maisha,  uwezo wa kubadilika kwa urahisi na kuzoea mazingira mapya, kujihisi salama na kujitambua.
 
Afya ya mtu na ya jamii kwa ujumla inaathiriwa na masuala mengi tofauti. WHO inaeleza kwamba, afya mbaya au nzuri ya watu inategemea mazingira wanayoishi, matukio 
 
yaliyowakumba katika maisha yao ya zamani na ya hivi sasa. Shirika hilo la Afya Duniani linatujulisha kuwa, masuala yafuatayo huweza kuathiri afya zetu kwa kiasi kikubwa na 
 
matumizi ya vituo vya afya katika jamii. Masuala hayo ni mahali tunapoishi, hali ya mazingira tuishiyo, jenetiki, kipato chetu, kiwango cha elimu zetu na uhusiano wetu na marafiki na familia.  WHO pia inasema, afya zinaainishwa na masuala makuu matatu,

Uchumi na jamii zetu au mazingira ya kijamii na kiuchumi.Mahala tunapoishi au yale yanayotuzunguka yaani mazingira ya kifizikia. Jinsi tulivyo na yale tunayoyafanya, yaani sifa na tabia binafsi ya mtu.
 
Kwa kuwa afya nzuri inategema mukhtadha wa maisha yetu, si sawa kusifu au kuwalaumu watu kutokana na afya mbaya au nzuri walizonazo.
 
Sababu kuu zinazochangia hali zetu za afya kuwa nzuri au mbaya mara nyingi haziko katika mikono wala uwezo wetu. 
 
Kwa mujibu wa WHO, miongoni mwa sababu hizo ni, hali ya kiuchumi na kijamii ambapo watu ambao wanaishi katika hali iliyoimarika kisiasa na kijamii, huwa na hali nzuri za kiafya kuliko wale wanaoishi kwenye jamii yenye hali mbaya ya kisiasa na kijamii.
 
 
Uhusiano huo unabainishwa wazi katika utafiti uliofanywa nchini Australia unaoonesha kwamba, wanawake wanaoishi kwenye jamii zenye hali duni kijamii na kiuchumi, mara nyingi hushindwa kuwanyonyesha watoto wao wachanga, suala ambalo huathiri afya za watoto hao.

 
Pia utafiti uliofanyika Korea Kusini umeonyesha uhusiano wa moja kwa moja kati ya hali duni ya kijamii na kiuchumi na hatari ya kupatwa na baadhi ya magonjwa kama mshituko wa moyo.

 
Elimu ni sababu nyingine inayoathiri afya zetu. Watu wasiokuwa na elimu ya kutosha kwa ujumla huwa hawana ufahamu mzuri kuhusiana na masuala yanayoathiri afya zao ikilinganishwa na wale walioelimika.
 
Utafiti uliofanywa na wataalamu katika Chuo Kikuu cha Tiba cha Feinberg huko Chicago Marekani umebainisha kwamba, watu wazima waliokuwa na kiwango cha juu cha elimu kuhusiana na masuala ya afya, wana nafasi kubwa ya kuishi maisha marefu kuliko kinyume chake.  

 
Suala jingine linaloathiri afya ni ajira. Takwimu zinaonesha kuwa, iwapo una kazi, basi una nafasi nzuri zaidi ya kuwa na afya bora kuliko mtu asiyekuwa na kazi. Kama una ajira ya kudumu na kazi nzuri zaidi, hali ya kiafya pia huboreka.
 
Hivyo ninahitimisha Makala hii ya AFYA NINI,
kwa usemi wa Mahatma Ghandi kuhusiana unaosema kwamba, "utajiri wa kweli ni uzima, na wala sio vipande vya dhahabu au shaba."

0 comments:

Post a Comment