Friday 7 November 2014

VYAKULA MUHIMU KWA WAJA WAZITO-2

Wiki iliyopita tuliona orodha ya vyakula hatari kwa wajawazito. Orodha hiyo imekatazwa kuliwa na wajawazito kwa sababu ina madhara kwa afya ya mtoto. Darasa hili ni muhimu kama mama anahitaji kuzaa mtoto mwenye afya na akili timamu.

Baada ya kujua orodha ya vyakula visivyofaa kwa wajawazito, wiki hii tujifunze vyakula vinavyofaa kuliwa zaidi na wajawazito. 

Kumbuka kwamba vyakula vyote vinaweza kuwa ni muhimu mwilini lakini huzidiana kulingana na mahitaji na hali ya mtu kwa wakati maalumu.

Mahitaji ya madini na vitamini mwilini wakati wa ujauzito huwa ni makubwa, hususani madini ya kashiamu, chuma na Vitamin B9 (folic acid).

MADINI YA KALISI (Calcium)
Wakati wa ujauzito, madini mengi ya kalisi husafirishwa kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kwa ajili ya kuimarisha mifupa na meno. Katika kipindi cha miezi sita ya mwanzo, mama huhifadhi madini hayo mwilini mwake. Kiumbe kinapokamilisha umbo lake katika kipindi cha miezi mitatu ya mwisho, hifadhi hiyo huanza kutumiwa na kiumbe hicho, hivyo mahitaji yake kuongezeka.

Katika kipindi hiki, mjamzito anatakiwa kula kwa wingi vyakula vinavyoongeza madini ya kalisi kama vile maziwa na vyakula vitokanavyo na maziwa. Kukiwa na upungufu wa madini hayo, meno ya mama na mifupa huathirika pia.

MADINI YA CHUMA (Iron)
Mahitaji ya madini ya chuma nayo huwa makubwa kwa wajawazito. Madini hayo ni muhimu kwa utengenezaji wa damu ambayo huhitajika kwa wingi na mama pamoja na mtoto.

Madini joto hupatikana kwa kula kwa wingi vyakula kama vile nyama, samaki, mayai, vyakula vilivyopikwa kwa nafaka zisizokobolewa (ugali wa dona, mkate mweusi, n.k) na mboga za majani kama vile spinachi na brokoli. Ili kupata madini hayo ya kutosha kutokana na vyakula hivyo, inashauriwa mjamzito kutumia pia vidonge vya Vitamin C (Vitamin C food supplements).

VITAMIN B9 (Folic Acid)
Vitamini hii ni muhimu sana kwa mjamzito, ni kosa kubwa sana la kiafya kwa mjamzito kuwa na upungufu wa vitamin hii. Vitamin B9 ndiyo inayohusika na ukuzaji na uimarishaji wa mfumo wa fahamu wa kiumbe tumboni. 

Aidha, Vitamin hii ndiyo inayotoa kinga ili viungo vya mtoto visiathirike na kuepusha uzaaji wa watoto walemavu au wenye kasoro za viungo kama ‘midomo ya sungura’ na kadhalika.

Vyakula vyenye kiwango kikubwa cha Vitamin B9 ni pamoja na mboga za majani, juisi ya machungwa, mapeasi, vyakula vilivyopikwa kwa ngano na mchele (hasa brown rice) na mayai. 

Hata hivyo, kutokana na hali ya vyakula vyetu, mjamzito hawezi kupata kiwango kinachotakiwa cha vitamin hiyo kwa kula vyakula peke yake.

Ili kupata kiwango cha vitamin hiyo kinachotakiwa, mjamzito atatakiwa kutumia pamoja na vidonge vya lishe vya Vitamin B9 ili kuepuka upungufu huo. Inashauriwa kutumia vidonge hivyo miezi michache kabla ya kushika mimba na katika kipindi cha miezi mitatu ya mwisho ya ujauzito, kipindi ambacho vitamin hiyo huhitajika kwa wingi.

Kwa ujumla, lishe bora ni muhimu kwa mjamzito katika kipindi chote cha ujauzito wake. Matatizo mengi ya kuzaa watoto wenye ulemavu wa aina mbalimbali, hutokana na upungufu wa madini na vitamin muhimu mwilini katika kipindi cha ujauzito. 

VYAKULA VINAVYOONGOZA KUONGEZA AKILI KWENYE UBONGO



BILA shaka ubongo ni miongoni mwa viungo muhimu vya binadamu lakini ni watu wachache sana wanaoutilia maanani. Ubongo ndiyo kiungo kinachohusika na utendaji kazi wote wa mwili na ndiyo unaowezesha mwili kuishi maisha ya furaha au karaha.
Hata hivyo, wakati mwingine utendaji kazi wa mwili unaweza kuwa siyo mzuri kutokana na sababu mbalimbali zinazoathiri ubongo, mojawapo ikiwa ni kukosekana kwa lishe bora na staili ya maisha inayotakiwa kuimarisha ufanisi wa ubongo.
Chakula ni moja ya sababu za msingi kabisa za kuimarisha ufanisi wa ubongo na kuzuia magonjwa mengine ya akili. Lakini kwa bahati mbaya watu wengi hawajui wale vyakula gani kwa lengo la kujenga akili na kuimarisha ubongo.
Ifuatayo ni orodha ya vyakula ambavyo vinaongoza kwa kuimarisha utendaji kazi mzuri wa ubongo:
MAFUTA YA SAMAKI
Mafuta ya samaki ni muhimu kwa ubongo na mfumo wa fahamu. Ulaji wa samaki wenye minofu kama samoni (salmon) na dagaa, utaweza kupata faida hizo kwa sababu aina hii ya samaki ina kiasi kingi cha mafuta ya Omega 3 ambayo huimarisha utendaji kazi na mawasiliano kati ya ubongo na seli za mwili moja kwa moja.
PILIPILI KALI
Pilipili kali nayo huwa ni chakula kikubwa cha ubongo kwa sababu ina kiwango kingi cha Vitamin C ambayo huhitajika zaidi kwenye ubongo, pilipili inaaminika kuwa na kiwango kingi cha vitamin hiyo kuliko hata machungwa.
MBEGU ZA MABOGA
Mbegu za maboga zina kiwango kingi cha madini ya ‘Zinc’ ambayo husadia kuongeza kumbukumbu (memory). Kuna njia nyingi za kula mbegu za maboga, moja wapo ni kuzikaanga na kula kama karanga, ukila kiasi cha kiganja kimoja kwa siku, inakuwa poa.
NYANYA
Nyanya ni muhimu sana kwa sababu huzuia magonjwa ya ubongo (brain disease) kutokana na kuwa na kirutubisho aina ya ‘Lycopene’ chenye uwezo wa kuzuia magonjwa nyemelezi yanayoweza kutokea. Hivyo ulaji wa nyanya utakusaidia kukupa kinga dhidi ya magonjwa mbalimbali, yakiwemo ya akili.
BROKOLI
Brokoli ni mboga ya majani aina fulani kama maua ya maboga, ambayo nayo inafaida sana kwenye ubongo, ina vitamin K, C na inatoa kinga ya mwili. Vitamin K inahusika moja kwa moja na utendaji kazi mzuri wa ubongo na husaidia kuzuia magonjwa yatokanayo na uzee.
KARANGA
Aina zote za karanga zina vitamin E, ambayo huzuia tatizo la upotevu wa kumbukumbu na pia zina mafuta yenye afya yanayohitajika mwilini.
MAYAI
Mwisho ni mayai ya kuku, ambayo yana kirutubisho aina ya Choline. Kirutubisho hiki huzalishwa mwilini kwa kiwango kidogo tu, hivyo kwa kula mayai (ya kienyeji) utaweza kuongeza kiwango cha kirutubisho hicho mwilini kwa kiwango kikubwa na hivyo kuimarisha afya ya ubongo.

Monday 3 November 2014

UGONJWA WA TUNDU KATIKA MOYO KWA WATOTO


Leo tutazungumzia ugonjwa unaojulikana kama tundu katika kuta za ventrikali za moyo au kwa kitaalamu Ventricular Septal Defect (VSD).
Tatizo hili hutokea mara nyingi ambapo watoto 2-6 kati ya 1,000 uzaliwa nalo.
Tundu katika kuta za chini za moyo au VSD ni pale panapokuwepo na uwazi katika sehemu ya kuta ya septum inayotenganisha chemba za ventrikali zilizo chini ya moyo.
Moyo unapoanza kuumbika huanza kama bomba lililo wazi na kuendelea kujigawa katika sehemu mbalimbali na kuunda kuta.
Iwapo kitendo hicho hakitatekelezwa ipasavyo, hutokea uwazi katika kuta ya septum kwenye chemba za chini.
Kuwepo tundu hilo huruhusu damu yenye oksijeni kupita kutoka chemba ya kushoto ya chini ya moyo na kuingia katika chemba ya kulia ya chini ya moyo, badala ya kuingia kwenye mshipa wa aorta na kuelekea nje ya moyo kama inavyotakiwa.
Tundu la VSD linaweza kuwa dogo, la kati au kubwa. Tundu dogo katika kuta za chini za moyo huruhusu damu ndogo tu kutoka upande mmoja wa moyo kwenda wa pili hivyo haliathiri utendaji wa kawaida wa moyo na kwa kawaida huwa halihitaji matibabu maalumu.
Matundu ya aina hiyo huziba yenyewe wakati moyo unapoendelea kukua kipindi cha utotoni. Matundu yenye ukubwa wa kati na kubwa katika kuta za chini za moyo huruhusu kiwango kikubwa zaidi cha damu kupenya toka upande mmoja wa moyo kwenda mwingine, na mara nyingi huhitaji matibabu maalumu.
Watoto wenye tundu dogo katika moyo, huweza kukua bila matatizo yoyote, wakati wale wenye tundu kubwa huanza kuonyesha dalili mapema.
Vifuatavyo ni vihatarishi ambavyo vinaweza kusababisha mtoto kuzaliwa na tundu katika kuta za chini za moyo. Mama kuwa na maambukizi ya Rubella katika kipindi cha ujauzito au kuwa na ugonjwa wa kisukari cha wakati wa ujauzito ambao haujadhibitiwa na kuwa mnywaji wa pombe au mtumiaji wa madawa ya kulevya.
Mjamzito akitumia bila ushauri wa daktari baadhi ya dawa za hospitali katika kipindi cha ujauzito pia huweza kusababisha mtoto azaliwe na tundu katika kuta za chini za moyo.
DALILI
Iwapo tundu ni dogo huwa halina dalili yoyote na pale mtoto anapoendelea kukua tundu hilo hujifunga lenyewe. Lakini tundu likiwa kubwa, japokuwa mtoto anayezaliwa huwa haonyeshi dalili yoyote katika kipindi  hicho lakini baadaye huwa na dalili zifuatazo.
Rangi ya ngozi yake, midomo na kucha hubadilika na kuwa ya bluu, kunyonya au kula huwa kwa shida sana, ukuaji na kupumua kwa shida, kuchoka haraka, kujaa miguu na kuvimba tumbo, kuwa na mapigo ya moyo ya haraka.
Mtoto mwenye tatizo hili anapopimwa na daktari kwa kifaa, huweza kusikia ishara ya ongezeko la sauti ya ziada ya mapigo ya moyo wa mtoto hali ambayo kitaalamu huitwa holosystolic murmur.

UGONJWA WA TUNDU KATIKA MOYO KWA WATOTO-2



MADHARA YA TUNDU KATIKA MOYO
Madhara ambayo yanaweza kusababishwa na tundu katika kuta za chini za moyo ni Eisenmenger syndrome, hali ambayo hutokea pia pale mtu anapokuwa na tundu katika kuta za juu za moyo.
Tatizo hili hutokea wakati mtiririko wa damu unapoongezeka kutoka kushoto kwenda kulia kupitia tundu katika kuta za moyo, suala ambalo huongeza mtiririko wa damu katika mishipa ya mapafu na kusababisha shinikizo la damu katika mapafu.
Hali hii husababisha ongezeko la shinikizo la damu katika upande wa kulia wa moyo na kubadilika kwa shanti kutoka kulia kwenda kushoto.
Matokeo yake ni kuwa damu isiyo na oksijeni iliyotakiwa kwenda kwenye mapafu kwa ajili ya kusafishwa huchanganyika na damu yenye oksijeni iliyoko upande wa kushoto na kusambaa mwilini.
Madhara mengine ya tundu la VSD ni kupata ugonjwa wa kiharusi, moyo kushindwa kufanya kazi vizuri pia maambukizi katika kuta za ndani za moyo (endocarditis) ugonjwa ambao tutauelezea katika matoleo yajayo.
Akinamama waliozaliwa na tatizo hili, ambao wametibiwa na hawakupata madhara wanaweza kushika mimba na kupitisha kipindi cha ujauzito bila matatizo yoyote.
Isipokuwa wale ambao hawakutibiwa au ambao tayari wameshapata madhara, hushauriwa kutoshika ujauzito kwa sababu ya hatari zinazoweza kutokea katika kipindi cha ujauzito.
Vilevile kwa akinamama waliozaliwa na tatizo hili, uwezekano wa watoto wao kuzaliwa na tatizo hili huwa mkubwa.
TIBA
Inafaa kujua kuwa, karibu nusu ya wagonjwa wenye tatizo hili huwa hawahitaji matibabu ya aina yoyote ile kwa kuwa tatizo hili hujirekebisha katika miaka ya mwanzo ya maisha yao.
Hata hivyo, kwa wale ambao watahitaji matibabu, hutibiwa kwa dawa au upasuaji kwa kutegemea ukubwa wa tatizo lenyewe.
Dawa zinazotumika kutibu ugonjwa huu ni zile ambazo hupunguza kasi ya moyo, huongeza nguvu ya mapigo ya moyo na zile ambazo hupunguza maji mwilini au diuretics.
Utaratibu wa kuziba tundu umegawanyika katika sehemu mbili na hufanyika iwapo tundu ni kubwa sana, au halikujirekebisha lenyewe wakati mtoto alipokuwa anakua na pale ikiwa dawa alizopewa mgonjwa hazikusaidia.
Pale inapohitajika upasuaji, mgonjwa hufanyiwa oparesheni ambapo kifua hufunguliwa ili kuziba tundu la VSD.
Matibabu mengine ni kupitisha mrija katika mshipa wa damu hadi katika sehemu ya tatizo kwenye moyo na kuliziba kwa kutumia kifaa maalumu. Kwa njia hii, huwa hakuna haja ya kufanya upasuaji wa kufungua kifua cha mgonjwa.
MWISHO

KUTOKWA NA MAJIMAJI SEHEMU ZA SIRI



Tatizo hili huwatokea wanawake na wanaume. Mwanaume hutokwa na majimaji katika njia ya mkojo, mwanamke hutokwa na majimaji haya katika njia ya mkojo au ukeni.
Majimaji haya yanaweza kuwa mepesi au mazito, pia yanaweza kuwa ni usaha kutegemea na chanzo cha tatizo.
Mwanaume mwenye tatizo hili, majimaji yanaweza kutoka yenyewe na kujikuta amechafua nguo za ndani au asubuhi anapoamka anajikuta amechafuka.
Wakati mwingine unapojisaidia haja kubwa majimaji haya hutoka kama manii yakiwa yanateleza toka katika njia ya mkojo.
Kwa upande wa mwanamke, kutokwa na majimaji haya inategemea ni wakati gani, aidha wakati wa ujauzito au wakati ambao siyo wa ujauzito.
Hali hii ikitokea wakati wa ujauzito siyo dalili nzuri, wakati mwingine huhatarisha hali ya ujauzito. Katika kipindi ambacho siyo cha ujauzito, tatizo hili linapotokea huwa na vyanzo vingi.
Jinsi tatizo linavyotokea
Mwanaume mwenye tatizo hili, kama anatokwa na usaha, utakuwa na historia ya kufanya ngono zembe siku za nyuma na siyo muda mrefu sana. Endapo utakuwa na majimaji mepesi itategemea kama yanawasha au la, kama hayawashi basi aidha utakuwa una tabia ya kujichua au ulishawahi kuumia njia ya mkojo.
Majimaji yanapotoka na kuhisi muwasho katika njia ya mkojo, inaashiria maambukizi sehemu hiyo yanayoweza kusababishwa na Fangasi, Klamidia na Trikomonia.
Hali hii pia inaweza kuwatokea hata wanawake ambao wanaweza kupata matatizo ukeni na katika njia ya mkojo kama inavyojielezea hapo juu.
Mwanamke kutokwa na uchafu mzito ukeni inategemea na chanzo, aidha inaweza kusababishwa na mabadiliko ya mwili au maambukizi. Hali hii inategemea na uchafu au majimaji hayo yapo katika hali gani.
Mwanamke mjamzito na asiye mjamzito endapo atatokwa na uchafu mzito ukeni ambao hauna harufu wala muwasho, hilo siyo tatizo na maambukizi, ni mabadiliko tu ya mwili. Kwa mwanamke ambaye siyo mjamzito, hali hii inaashiria kutopevusha mayai na hawezi kupata ujauzito.
Uchafu wenye rangi aidha njano, rangi ya udongo au damu, au unatoa harufu, basi ni tatizo linalohitaji uchunguzi wa kina.
Dalili za tatizo
Kama nilivyoelezea jinsi tatizo linavyotokea, hali ya kutokwa na uchafu au majimaji ukeni huambatana aidha na muwasho, harufu au la.
Kama hakuna harufu au muwasho hali inapotokea kwa mwanamke tatizo linaweza kuwa katika mfumo wa homoni na hali inapotokea ikaambatana na muwasho harufu tatizo ni maambukizi.
Maambukizi yanaweza kuwa Kisonono au Gono, Kaswende, Klamidia, Trikomonia na Fangasi.
Matatizo haya yanaweza kuambatana na  maumivu katika njia ya mkojo, chini ya tumbo na kiuno kwa wanaume na hata kuathiri uwezo wa kufanya tendo la ndoa.
Kwa wanawake tatizo linaweza kuambatana na maumivu katika njia ya mkojo, maumivu ukeni, maumivu wakati wa tendo la ndoa, maumivu chini ya tumbo na maumivu ya kiuno.
Mwanamke pia hupoteza hamu ya tendo la ndoa, mzunguko wa hedhi huvurugika, kutopata ujauzito na kupoteza hamu ya tendo la ndoa. Matatizo haya humfanya mgonjwa apoteze hamu ya kula na mwili kuwa mchovu na kukosa raha.
Uchunguzi
Hufanyika katika kliniki za magonjwa ya kinamama. Muone daktari bingwa wa kinamama kwa uchunguzi wa kina.
Vipimo vipo vya aina nyingi kama vya damu, kupima shingo na mdomo wa kizazi, kupima uchafu utokao ukeni, kipimo cha Ultrasound na vingine ambavyo daktari ataona vinafaa.

FANYA MAMBO 5 ILI UWEZE KUJIKINGA NA MARADHI.



 1. Jitahidi kadiri uwezavyo kufanya mambo haya matatu: kula vizuri, kufanya mazoezi ya kutosha, na kupumzika vya kutosha.
 
 2. Dumisha usafi. Wataalamu wa afya husema kwamba kunawa mikono ndiyo njia bora ya kujikinga na magonjwa au kuepuka kueneza maambukizo.
 
 3. Hakikisha kwamba chakula mnachokula na familia yako ni salama. Hakikisha mikono yako na mahali unapotayarishia chakula ni safi. Pia, hakikisha kwamba unatumia maji safi kunawa mikono na kusafisha chakula. Kwa kuwa viini huzaana ndani ya chakula, pika nyama kabisa. Hifadhi vyakula vizuri.
 
 4. Katika maeneo ambayo magonjwa hatari huenezwa na wadudu wanaoruka, epuka kuwa nje usiku au mapema asubuhi wakati ambapo wadudu ni wengi. Jikinge kwa chandarua sikuzote.
 
 5. Kupata chanjo kunaweza kuimarisha mfumo wako wa kinga ili upambane na viini vinavyopatikana mahali unapoishi.

SABABU ZA TATIZO LA KUTOPATA MIMBA - 3



Kipimo cha upevushaji wa mayai kupima mirija ya uzazi, upasuaji mdogo kwenye tumbo na kumulika ndani ya mwili wake pia kipimo cha Ultrasound kitafanyika.
Vipimo kwa upande wa wanaume
Baada ya kuchukuwa historia  ya mgonjwa kwa urefu  kinachofuata ni vipimo vya kuangalia kama yupo kawaida  au kama kuna hitilafu. Vipimo hivyo ni kumchunguza  mwanaume kwa ujumla hali ya afya yake kwa kumpima kuanzia kichwani hadi miguuni.
Kupima mbegu zake,  kupima vichocheo vyake vya uzazi, kupima na Ultrasound kwenye korodani zake.
Ushauri 
Muda wa kufanya   Mwanamke anashauriwa kulalia mgongo huku ameinua magoti baada ya kufanya tendo la ndoa kwa muda wa dakika 20.
Kutotumia mafuta yoyote ya kulainisha uke kwani baadhi ya mafuta huua mbegu za kiume.
Kuacha kuvuta sigara kwa mwanaume na mwanamke  kwani uchunguzi huonyesha  kuwa uvutaji wa sigara  unasababisha ugumba na utasa.
Kupunguza uzito kwa mwanamke na mwanaume na kutumia vidonge vya madini  ya foric acid kwa ushauri wa daktari kumeonyesha msaada mkubwa kwa akina mama wanaopata shida ya kupata mimba.
Upimaji wa mbegu za kiume
Mbegu za kiume baada ya kutolewa zinatakiwa kufikishwa maabara kabla ya dakika 30 kwa upimaji.
Mwanaume anashauriwa kukaa siku 3 bila kufanya tendo la ndoa ndipo atoe mbegu zake. Ujazo au wingi wa mbegu kawaida ziwe zaidi ya milioni mbili. Kwa kawaida wingi wa mbegu ni zaidi ya milioni 25.

SABABU ZA TATIZO LA KUTOKUPATA MIMBA-2


Leo nitaelezea matibabu na ushauri kwa wanandoa wanaokabiliwa na tatizo la mama kutopata mimba.
Miongoni mwa mambo wanayopaswa kuelezwa  wanandoa hao ni kuwapa uzoefu kuhusiana na afya ya uzazi na jinsi ujauzito unavyoweza kupatikana na hatimaye kupata mtoto.
 Pia kuona jinsi ya  kuunganisha familia na kujenga familia bora kama itashindikana kupata mtoto bila mume kumtenga mke au mke kumtenga mume.
Kutumia muda mwingi wa kufuatilia kliniki bila kuchoka na kutumia kiasi cha muda wao kushughulikia uzazi.
Njia tofauti za matibabu (Fertility treatment options)
-Kuhakikisha mayai ya mwanamke yanapevuka.
-Kurekebisha mirija na matatizo ya mji wa mimba kama kuondoa uvimbe.
-Matibabu ya mwanaume mwenye matatizo ya mbegu.-Njia ya kupandikiza mbegu (Assisted reproductive technology).  Dawa zinazotumika kupevusha mayai ni kama Clomiphene citrate, letrozole, tamoxifen, progynora, Inj HCG inj, vaginal progesterone, Human menopausal gonadotropin, FSH, GN-RH, metformin, Bromocriptine, dawa hizi zinasaidia sana kurutubisha mayai bila kuleta madhara yoyote kwa mtumiaji, matatizo ambayo yanaweza kujitokeza ni kama kuzaa mapacha, wakati wa utumiaji wa dawa hizi ni lazima daktari awe mwangalifu wa kuangalia vipimo kama vile damu (vichocheo hormone) Ultrasound kuangalia kifuko cha mayai.
Njia nyingine zinazotumika katika matibabu ni njia ya upasuaji kama vile oparesheni ndogo tumboni kumlika uzazi (laporoscopic techniques).
Kifuko cha uzazi (ovaries) na kuchukua mbegu za mwanaume na kuziunganisha kwenye kifaa maalum (maabara hatimaye kuingiza kwenye mji wa mimba kwa kutumia vifaa maalum kama bomba la sindano.
Mama mhusika anayetakiwa kupandikiza ni lazima asiwe na umri usiozidi miaka 40.

MAAJABU YATOKANAYO NA MFUMO WA MZUNGUKO WA DAMU MWILINI



Maajabu ya Mfumo wa Mzunguko wa Damu
WAZIA nyumba yenye mfumo tata wa mabomba kiasi cha kwamba kioevu kinachopitia humo kinaweza kusafirisha chakula, maji, oksijeni, na uchafu kwa njia salama. Isitoshe, mabomba hayo yanaweza kujirekebisha ili kumudu mahitaji mbalimbali nyumbani. Huo ungekuwa uhandisi bora kama nini!
Lakini, “mabomba” ya mwili wako hufanya mengi zaidi. Mbali na kudumisha halijoto ya mwili wako, husafirisha pia homoni nyingi sana, au chembe zinazosafirisha kemikali, na kingamwili dhidi ya maradhi. Mfumo wote ni laini na hunyumbulika pia, na hivyo huweza kustahimili mshtuko na kunyumbulika na viungo vya mwili. Mfumo huo haungeweza kubuniwa na mhandisi yeyote mwanadamu, lakini ndivyo alivyofanya Muumba alipoumba vena, ateri, na kapilari za mwili wa mwanadamu.

Sehemu za Msingi za Mfumo Huo
Kwa kweli mfumo wa mzunguko wa damu wa mwanadamu ni mifumo miwili inayofanya kazi pamoja.
  • Mmoja ni mfumo wa mishipa ya damu ya moyo, ambao umejumuisha  

    moyo, damu, na mishipa yote ya damu.
  • Mwingine ni mfumo wa limfu—mfumo wa mishipa inayosafirisha maji ya ziada, yanayoitwa limfu, kutoka kwa tishu za mwili na kuyarejesha kwenye damu. Mishipa ya damu ya mtu mzima mmoja tu ikiweza kuunganishwa kwa mstari ulionyooka, inaweza kufikia umbali wa kilometa 100,000 na hivyo kuizunguka dunia mara mbili na nusu! Mfumo huu wenye kuenea sana husafirisha damu ya uhai, inayofanyiza asilimia 8 hivi ya uzito wa mwili, hadi kwenye mabilioni ya chembe.
Bila shaka, moyo ndio chanzo cha nishati inayoendesha mfumo wa mishipa ya damu ya moyo. Unalingana na ngumi yako, nao husukuma angalau lita 9,500 za damu kila siku katika mwili wako wote—kwa ujumla ni kama kuinua uzani wa tani moja kwa kimo cha meta kumi kila muda wa saa 24!

Kuuchunguza Mfumo wa Mishipa ya Damu ya Moyo
Damu huzungukaje? Acheni tuanze na damu isiyo na oksijeni inayoingia katika moyo kupitia vena mbili kubwa—vena kubwa (ya juu) na vena kubwa (ya chini). (Ona picha.) Vena hizo hupeleka damu kwenye chumba cha kwanza cha moyo, chumba cha juu cha kulia (rightatrium). Chumba cha juu cha kulia husukuma damu kwenye chumba chenye misuli zaidi, chumba cha chini cha kulia (right ventricle.) Kutoka humo damu huenda mapafuni kupitia shina la mapafu na ateri mbili za mapafu—ateri pekee zinazosafirisha damu isiyo na oksijeni. Kwa kawaida damu hiyo husafirishwa na vena.

Mapafu huondoa kaboni dioksidi na kutia oksijeni katika damu hiyo. Kisha damu hutiririka kwenye chumba cha juu cha kushoto cha moyo (left atrium) kupitia vena nne za mapafu—vena pekee zinazosafirisha damu iliyokolea oksijeni. Chumba cha juu cha kushoto huelekeza damu hiyo katika chumba cha moyo chenye msukumo wenye nguvu zaidi, chumba cha chini cha kushoto (left ventricle), humo damu iliyokolea oksijeni husambazwa mwilini kupitia aorta (ateri kubwa). 

Vyumba viwili vya juu vya moyo hufumbuka pamoja kisha vyumba vya chini hufumbuka, utendaji huo wa pamoja hutokeza pigo la moyo. Vali nne za moyo huruhusu damu kusonga mbele moyoni bila kurejea nyuma.

Chumba cha chini cha kushoto chenye misuli zaidi huwa na msukumo unaozidi ule wa chumba cha chini cha kulia kwa mara sita, kwa sababu chumba cha chini cha kushoto husukuma damu katika mwili mzima. Msukumo huo ungeweza kwa urahisi kusababisha uvimbe (kuvimba au kupanuka kwa kuta za ateri) au hata kiharusi hatari ubongoni endapo hakungekuwa na utaratibu bora wa kupunguza msukumo huo wenye nguvu.

Ateri Zenye Kunyumbulika
Ateri kubwa zaidi mwilini mwako, aorta, na matawi yake makuu huitwa “ateri zenye kunyumbulika.” Sehemu yake ya ndani ni kubwa, ikiruhusu damu itiririke kwa urahisi. Zina kuta nene pia, zenye misuli zinazofunikwa na matabaka ya elastin, protini inayoshabihi mpira. Chumba cha chini cha kushoto 

kinaposukuma damu kwenye ateri hizo, zinapanuka au kuvimba, kisha hupunguza msukumo huo wenye nguvu sana na kusukuma damu hadi kwenye ateri, ateri zenye misuli au ateri zinazosambaza damu, ambazo pia zina kuta zenyeelastin. Msukumo wa damu huimarishwa na umbo hilo la ajabu kabla ya kufika katika kapilari (mishipa midogo) laini.*

Ateri zinazosambaza damu zina kipenyo cha kati ya sentimeta 1 hadi milimeta 0.3 hivi. Mishipa hiyo ya damu huelekeza mtiririko wa damu kwa kutunuka au kunywea kama zinavyoongozwa na nyuzinyuzi za pekee za neva, jambo hilo hufanya mfumo wa mzunguko wa damu utende kwa bidii sana. Mathalani, kunapotokea zahama au hatari, vipima-msukumo katika kuta za ateri huonya 

ubongo, kisha ubongo huwasilisha ujumbe kwa ateri zifaazo ili kupunguza mtiririko wa damu kwenye sehemu zisizo muhimu sana kama vile ngozi na kuielekeza kwenye viungo muhimu. Gazeti la New Scientist lasema hivi: “Ateri zako zaweza ‘kuhisi’ mtiririko wa damu, na kuitikia.” Je, si ajabu kwamba ateri zimetajwa kuwa “mabomba yenye akili”?

Kabla ya damu kutoka kwenye ateri ndogo zaidi—arterioles—msukumo wake huwa umeimarika kufikia milimeta 35 hivi za hidrajiri. Msukumo taratibu na imara, ni muhimu wakati huo kwa sababu ateri hizo ndogo sana huungana na mishipa midogo zaidi ya damu, kapilari.

Msururu wa Chembe Nyekundu
Zikiwa na kipenyo cha mikrometa nane hadi kumi, kapilari huwa nyembamba sana kiasi cha kwamba chembe nyekundu za damu hupenya kwa msururu. Japo kuta za kapilari huwa na tabaka moja tu ya chembe, huwa zinapitisha virutubishi (vinavyobebwa na plasma au umajimaji wa damu) na oksijeni 

(inayosafirishwa na chembe nyekundu) kwenye tishu zilizo karibu. Wakati huohuo, kaboni dioksidi na uchafu mwingine hutoka kwenye tishu na kukusanywa na kapilari ili ziondolewe mwilini. Kapilari zaweza pia kuelekeza mtiririko wa damu ikitegemea mahitaji ya tishu iliyo karibu, kupitia kwa msuli mdogo wenye umbo la kitanzi unaoitwa sphincter.

Kutoka kwa Vena Ndogo Kupitia kwa Vena Kubwa Hadi Moyoni
Damu inapotoka kwenye kapilari, huingia kwenye vena ndogo sana zinazoitwa venules. Vena hizo ndogo zenye kipenyo cha kati ya mikrometa 8 na 100, huungana kufanyiza vena ambazo hurejesha 

damu moyoni. Msukumo wa damu huwa umepungua sana inapofika kwenye vena, hivyo basi kuta za vena huwa nyembamba sana kuliko kuta za ateri. Pia zina kiasi kidogo chaelastin. Hata hivyo, sehemu yake ya ndani ni kubwa zaidi, hivyo hubeba asilimia 65 ya damu yote mwilini mwako.
Ili kushinda hali hiyo ya kupungua kwa msukumo wa damu, vena hurejesha damu moyoni kwa njia ya kustaajabisha sana. Kwanza, zina vali maalum zinazoshabihi vikombe ambazo huzuia damu 

kutiririka kutoka moyoni kwa sababu ya nguvu za uvutano. Pili, zinatumia misuli ya kiwiliwili cha mwili wako. Vipi? Misuli yako inaponyooka, tuseme katika miguu unapotembea, inabana vena zilizo karibu. Mbano huo husukuma damu kupitia vali zinazofunguka upande mmoja kuelekea kwenye moyo. Hatimaye, msukumo katika tumbo na katika kifua, unaosababishwa na kupumua, husaidia vena kusukuma damu kwenye chumba cha juu cha kulia cha moyo.

Mfumo wa mishipa ya damu ya moyo hufanya kazi kwa njia bora sana hivi kwamba hata mtu anapopumzika, unarejesha moyoni takriban lita 5 za damu kila dakika! Kutembea huzidisha kiasi hicho kufikia takriban lita 8, na mwanariadha mkakamavu aweza kuwa na lita 35 za damu zikibubujika kwenye moyo wake kila dakika—kiasi kinachozidi mara saba kile kiasi cha damu inayorejea moyoni mtu anapopumzika!

Nyakati nyingine vali za vena zinaweza kuvuja kwa sababu ya kasoro zilizorithiwa au kwa sababu mtu amenenepa kupita kiasi, au ni mja mzito, au mtu anaposimama kwa muda mrefu zaidi. Vali hizo zinapoziba, damu hufanyiza madonge chini yake, hilo huvimbisha vena na kusababisha ugonjwa wa kuvimba vena. Vivyo hivyo, kukaza misuli wakati wa kujifungua mtoto au wakati wa kwenda haja kubwa msalani, hubana sana tumbo, na hivyo damu hushindwa kurejea toka kwenye vena za mkundu na utumbo mpana. Hilo laweza kuvimbisha vena na kusababisha ugonjwa wa puru.

Mfumo wa Limfu
Kapilari hupeleka virutubishi kwenye tishu na kuondoa uchafu, lakini hukusanya maji machache sana kuliko yale ambayo zinasambaza. Protini muhimu za damu huvuja kwenye tishu. Ndiyo sababu mwili unahitaji mfumo wa limfu. Unakusanya maji yote ya ziada, yanayoitwa limfu, na kuyarejesha kwenye damu kupitia kwa vena kubwa iliyo chini ya shingo na nyingine iliyo kifuani.

Kama ilivyo na ateri na vena, kuna mishipa mbalimbali ya limfu. Mishipa midogo sana, inayoitwa kapilari za limfu, hufanyiza matabaka ya kapilari za damu. Mishipa hiyo midogo sana yenye kupenyeka kwa urahisi, hufyonza maji ya ziada na kuyapeleka kwenye mishipa mikubwa zaidi inayokusanya limfu na kuisafirisha kwenye mashina ya limfu. Mashina hayo huungana na kufanyiza vifereji vya limfu, vinavyopeleka limfu kwenye vena.

Limfu hutiririka upande mmoja tu—kuelekea kwenye moyo. Kwa hiyo, mishipa ya limfu haifanyizi mzunguko kama mfumo wa mishipa ya damu ya moyo. Utendaji dhaifu wa misuli ya mishipa ya limfu, pamoja na mpigo wa ateri zilizo ujiranini na kusogea kwa viungo, husaidia kusukuma maji ya limfu kupitia mfumo huo. Mishipa ya limfu inapoziba popote husababisha mrundamano wa maji kwenye sehemu iliyoathiriwa, hilo hutokeza uvimbe unaoitwa chovya.

Viini vya maradhi vyaweza pia kupitia kwenye mishipa ya limfu na kuingia mwilini. Kwa hiyo, Muumba wetu aliumba mfumo wa limfu ukiwa na kinga thabiti, viungo vya limfoidi: mafundo ya limfu—yaliyosambaa katika mishipa ambayo yanakusanya limfu—wengu, matezi ya dundumio, mafindifindo, kidole-tumbo, na folikali za limfoidi (Peyer’s patches), katika utumbo mwembamba. Viungo hivyo 

husaidia kutengeneza na kuhifadhi chembe za limfu ambazo ni chembe muhimu za mfumo wa kinga. Kwa hiyo, mfumo wa limfu wenye afya huchangia mwili wenye afya.

Hapa ndipo uchunguzi wetu wa mfumo wa mzunguko wa damu unapofikia tamati. Lakini, hata uchunguzi huu mfupi umefunua maajabu ya uhandisi yaliyo tata na bora zaidi. Isitoshe, mfumo huo hufanya kazi zake nyingi kimyakimya, bila wewe kujua—ila unapougua. Kwa hiyotunza mfumo wako wa mzunguko wa damu, nao utakutunza.



Mfumo wa Mishipa ya Damu ya Moyo
                                Damu iliyokolea oksijeni
             →   MAPAFU   →
MOYO                              MOYO
Chumba cha Chini Kulia           Chumba cha Chini Kushoto
   ↑                                 ↓
VENA                            ARTERI
   ↑                                 ↓
VENA NDOGO                       ATERI NDOGO
          ←   KAPILARI   ←
Damu isiyo na oksijeni
       Damu isiyo na oksijeni
    Kutoka mwilini                Kutoka mwilini
VENA KUBWA YA JUU         VENA KUBWA YA CHINI
        ↓                        ↓
              CHUMBA CHA JUU KULIA
                    ↓
             CHUMBA CHA CHINI KULIA
                   vali
                    ↓
                Hadi mapafuni
              ATERI YA MAPAFU
            Damu iliyokolea oksijeni
                Kutoka mapafuni
                    ↓
            CHUMBA CHA JUU KUSHOTO
                   vali
                    ↓
           CHUMBA  CHA CHINI  KUSHOTO
                    ↓
                  AORTA
                    ↓
                 Hadi mwilini

* Moyo ndio chanzo cha nishati inayoendesha mfumo wa mishipa ya damu ya moyo. Unalingana na ngumi yako, nao husukuma angalau lita 9,500 za damu kila siku katika mwili wako wote—kwa ujumla ni kama kuinua uzani wa tani moja kwa kimo cha meta kumi kila muda wa saa 24!

JINSI YA KUJIKINGA NA KUONDOA HARUFU MBAYA MDOMONI!


WATU wengi husumbuliwa na tatizo la kunuka mdomo bila hata kujijua hivyo kuwa kero kwa wenzao na wakati mwingine hujishushia hadhi mbele ya jamii. Mara nyingi ugonjwa wa kunuka mdomo (Halitosis) husababishwa na uchafu wa kinywa na ulaji wa vyakula usiosahihi lakini ni tatizo linalotibika.
Ni rahisi kulizuia na kuliondoa tatizo la kunuka mdomo iwapo utaamua kufuata kanuni za usafi wa kinywa na unywaji wa maji kwa kufuata kwa makini muongozo ufuatao:
KUPIGA MSWAKI
Kitu cha kwanza kufanya ni kupiga mswaki kwa ukamilifu kila uamkapo asubuhi. Wakati wa kupiga mswaki, utatakiwa siyo tu kusugua meno, bali pia ulimi, sehemu ya katikati hadi karibu na koromeo kwa kusugua vizuri.
Vile vile kila uamkapo baada ya kulala mchana au jioni, hakikisha unapiga mswaki, kwani bakteria wa kinywani, hutawala kinywa kila ulalapo. Mara baada ya kupiga mswaki na kusugua ulimi sawaswa, hakikisha unasukutua vizuri kwa maji, kwani hapa ndipo baadhi ya watu hukosea kwa kupiga mswaki bila kusukutua kwa maji.
KUNYWA MAJI MENGI
Maji ni muhimu sana karibu kila eneo la mwili wa binadamu. Unywaji wa maji ya kutosha kila siku utakusaidia kudhibiti na hatimaye kuondoa tatizo la kunuka mdomo. Unywaji wa maji mengi ni muhimu, hasa kwa wale watu wenye ugonjwa wa kukauka midomo (xerostomia).
Mara nyingi harufu itokayo mdomoni, hutokea tumboni na siyo kinywaji peke yake kama unavyoweza kudhani. Hivyo, kama tumbo litakuwa chafu, hata kama utasafisha kinywa vizuri bado harufu mbaya inaweza kuendelea kutoka.
Harufu mbaya ya tumboni hutokea pale tumbo linapokuwa chafu kutokana na kutopata choo kwa muda mrefu. Miongoni mwa mambo yanayochangia kukosekana kwa choo kwa muda mrefu ni pamoja na tabia ya kutokunywa maji ya kutosha kwa siku, hivyo hakikisha unakunywa maji, kiasi kisichopungua 

lita moja na nusu hadi mbili au zaidi, kutegemeana na kazi unazozifanya.
Ukiwa na tatizo la kukaukiwa maji mwilini kila mara, mwili hujaribu kutumia njia zake za kiasili kupunguza uzalishaji wa mate ili kuhifadhi maji kwa ajiili ya matumizi mengine, kitendo hicho huchangia kunukisha mdomo kwa sababu ndani ya mate huwa kuna kinga muhimu dhidi ya baktetria wanaonukisha kinywa.
Kwa upande mwingine, ili kuzuia kinywa kunuka pale mdomo unapokuwa umekaukiwa na mate, ni vizuri kutafuna vitu kama bazooka au ‘chewing gum‘ yoyote ili kuzalisha mate ambayo huhitajika katika kudhibiti bakteria.
Mwisho, hakikisha unasukutua sawaswa baada ya kula chakula chochote, hata kama ni juisi isipokuwa unapokunywa maji tu ya kawaida. Bila shaka, ukizingatia haya, tatizo ulilonalo la kunuka mdomo litataoweka na kubaki historia.